
Shirika lisilo la kiserikali la Forum for African Women Educationalists Tanzania. (FAWETZ) Lenye matawi yake Tanzania Bara na Visiwani, limetoa mafunzo yaTUSEME kwa wanafunzi wa shule ishirini na moja(21) Bara na Visiwani.
Tuseme ni programu inayomwezesha mwanafunzi wa kike na wa kiume, kujitambua na kuona umuhimu wa kuwa shuleni, ambao utasababisha kongezeka kwa mahudhurio shuleni, kupanda kwa Taaluma na kupunguza Mimba za utotoni pamoja na utoro.
Wakitoa mafunzo hayo katika Mkoa wa Shinyanga kwenye wilaya ya Shinyanga vijijini, na Kahama na kisiwa cha Pemba. Mratibu wa shirika hilo Bi Neema Kitundu, akiambatana na wawezeshaji Anne Balisidya, na Octavian Mgaya, walizifikia shule ishirini na moja, zilizo katika mradi wa “Safe space”(Mahali Salama) unaofadhiliwa na kuendeshwa na shirika la maendeleo ya elimu sayansi na utamaduni,(Unesco) Tanzania
Shule zilizonufaika na mafunzo yaTuseme katika wilaya ya Kahama ni shule ya sekondari Lunguya, Mwalugulu, Buliyanhulu, Mwalimu Nyerere Sekondari, Isaka Sekondari, Nyashimbi Sekondari na Kishimba Sekondari.
Aidha katika wilaya ya Shinyanga vijijini wanafunzi wa shule ya sekondari Pandagichiza, Usanda, Iselamagazi, Mwantini, Lyabukande, Ihugi na Tinde Day waliweza pia kunufaika na elimu hiyo.
Baada ya mafunzo hayo wanafunzi waliweka maazimio ya kutokukatisha masomo kwasababu zozotezile na kuhakikisha watafaulu katika masomo yao. Lakini pia watawapa elimu hiyo wanafunzi wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki.
Kwa upande wa Tanzania visiwani, shule saba zilizopo Pemba nazo pia zilipata elimu hiyo. Shule hizo ni pamoja na Shule ya sekondari Mgogoni, Micheweni, Chwakatumbe, Tumbe, Shumbavyamboni, Wingwi na Makangale.
Miongoni mwa changamoto zilizobainiwa kusababisha vikwazo kwa elimu ya wasichana na wavulana ni pamoja na wasichana kuozeshwa mapema, kupata ujauzito wakiwa shuleni, kupewa kazi nyingi nyumbani na umbali mrefu kutoka shuleni.
Kwa upande wa wavulana, changamoto wanazokutana nazo ni kuozeshwa mapema, kuchunga, kujitafutia mahitaji wenyewe, hasa baada ya kufiwa na wazazi wao na kwenda kuvua.
Ikiwa ni sehemu ya mafunzo haya ya TUSEME, yalifanyika maonyesho yaliyowashirikisha wazazi na walezi wa wanafunzi pamoja na wanafunzi na walimu wao, yaliyokuwa na lengo la kuibua mikakati shirikishi ya kuondoa vikwazo hivyo kwa pamoja yaani wanafunzi,waalimu na jamii inayozunguka shule kuunganisha jitihada ili kuwepo na elimu bora kwa manufaa ya watoto,wazazi na Taifa kwa ujumla.